WANATAALUMA WA MISITU WATAKIWA KUWA SULUHUSHO LA MIGOGORO KWENYE MIPAKA YA HIFADHI ZA MISITU

HOJA NEWS BLOG

Na Anangisye Mwateba-Arusha

Naibu Waziri wa Maliasili na utalii Mhe. Dunstan Kitandula (Mb) amewataka wanataaluma waliopo katika vyuo vya misitu kutumia taaluma za kupata suluhisho la migogoro ya mipaka kati ya hifadhi za misitu na makazi ya wananchi.

Mhe. Kitandula ameyasema hayo alipokuwa kwenye ziara ya kutembelea Taasisi ya Elimu ya Misitu Olmotonyi jijini Arusha na kuongeza kuwa wanataaluma hao wanategemewa na Taifa kutokana na maarifa wanayoyapata vyuoni. 


Aidha, Mhe. Kitandula  ameongeza kuwa kwa sasa wizara ya maliasili na utalii iko kwenye mkakati wa kuunganisha vyuo vyote vilivyo chini ya wizara ya maliasili ili viwe chini ya Chuo kimoja lengo likiwa ni kuboresha na kuleta tija kwa kile ambacho kinazalishwa na vyuo hivyo.

Vilevile Mhe. Kitandula ameendelea kuwakumbusha wanataaluma waliopo katika vyuo vilivyopo chini ya wizara ya Maliasili na Utalii kuandika maandiko yenye tija na ushawishi kwa serikali na wafadhili ili kuwa na miradi endelevu ya uhifadhi wa misitu na Wanyama.

Mkuu wa Chuo cha Misitu Dkt. Joseph Makero alimpongeza Mhe. Angellah Kairuki Waziri wa Maliasili na Maliasili na Naibu wake  kwa kazi kubwa wanayoifanya ya kuutangaza utalii na kuwa vinara  wa uhifadhi, na kwamba wao kama Chuo cha Misitu wamejipanga kuwaunga mkono na kuhakikisha dira na dhima ya Wizara inafikiwa.

Share this

Related Posts

Previous
Next Post »