MWENGE, kwa mujibu wa maana, ni kitu mfano wa kikombe chenye mpini mrefu
na utambi ambacho aghalabu huwasha na kukimbizwa katika kusheherekea au
kutukuza tukio fulani (Kamusi ya Kiswahili Sanifu, TUKI, OUP, ukurasa
wa 295 na Kamusi ya Karne ya 21, LONGHORN, ukurasa wa 375).
Mwenge unafanana sana na kibatari (koroboi) inayotumia mafuta ya taa. Hata hivyo, mwenge kwa wananchi wengi wa Tanzania ni ishara ya uhuru wa Tanganyika!
Imefanywa ishara, kama ilivyoashiriwa na Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, aliyetanganza azimio la kuwasha “mwenge wa uhuru.”
Historia inatukumbusha kwamba, Mwalimu Nyerere akihutubia Baraza la Kutunga Sheria [LEGICO] wakati huo, mnamo mwezi wa Oktoba 22, 1959 kama Mwenyekiti (Rais) wa TANU na mjumbe wa LEGICO, Mwalimu Nyerere alisema:
“Sisi (Watanganyika), tunataka kuuwasha mwenge na kuuweka juu ya Mlima Kilimanjaro, umulike hata nje ya mipaka yetu, ulete tumaini pale ambapo hakuna matumaini, upendo pale ambapo pana chuki, heshima ambapo pamejaa dharau.”
Haya yalikuwa maneno yenye “mvuto wa kisiasa,” “hamasa ya kijamii,” na “changamoto ya kiuchumi” kwa kizazi cha vijana wa Tanganyika (wakati ule na enzi zile). TANU ilipokea maneno haya na kuyatumia kama “chachu” ya kuleta mabadiliko.
Dhana ya mwenge, ukiachilia mbali historia na falsafa ya matumizi yake, kwenye maeneo aliyokulia Mwalimu Nyerere (yaani, Butiama ambako ibada ya mwenge ilikuwa sehemu ya matambiko ya wenyeji wa huko) ilikuwa kichocheo katika dhana ya uhuru.
Maneno yaliyotumiwa na Mwalimu Nyerere katika kuweka jiwe la msingi la kuwasha mwenge yalikuwa ndio falsafa iliyowaleta Watanganyika chini ya chama ukombozi (TANU) katika kupigania uhuru kwa moyo wa kizalendo na kujitolea kwa hali na mali.
Vijana, kama sehemu muhimu ya harakati za ukombozi kwa kutumia TANU walichukua alama ya “mwenge” na kuifanya alama yao. Vijana wa TANU (TANU Youth League, TYL) waliufanya mwenge kuwa dira ya maisha ya vijana.
Hata sasa, na kwa mujibu wa ushahidi wa kadi za Umoja wa Vijana wa CCM, mwenge umeendelea kuwa “Alama ya UVCCM.” Hata hivyo, mada hii ya wiki haiandikwi katika kutafuta nani anamiliki nini na kwa nini kwenye mwenge wa uhuru; isipokuwa ni katika kuwakumbusha wapanga sera kwamba, “falsafa ya mwenge imepoteza maana.” Mwenge haikuwashwa ili ukimbizwe kama upepo unaofuata mwelekeo na kamwe haurudi nyuma! Dhana ya kukimbiza mwenge si falsafa ya kukimbia kutoka ulipowashwa kuelekea utakakozimwa; hasha! Utakuwa ni ujinga kudhani kwamba, “mwenge ni kuuwasha na kuukimbiza huku ukifungua miradi ya pwagu na pwaguzi.” Dhana ya mwenge haiwezi kupimwa kwa mikesha, sherehe na kupita kila pembe ya nchi.”
Tuanze na nukta ya kwanza; matumaini. Mwenge uliwashwa ili ulete tumaini pale pasipokuwa na matumaini. Suala muafaka la kuuliza hapa ni: matumaini gani mwenge uliwashwa kwayo? Jibu rahisi (na la haraka) ni: uhuru! Falsafa ya uhuru haiwezi kupimwa kwa kutokuwapo kwa wakoloni. Uhuru wa maamuzi ndio lililokuwa lengo la harakati za ukombozi na kujikomboa kutoka kwa utawala wa Uingereza ambao uliweka wasaidizi wake (Gavana) na watendaji wengine waliyewakilisha masilahi ya ukoloni. Uhuru uliyodhamiriwa ni ukombozi wa fikra za kujitawala.
Mwongozo wa TANU wa 1971 ukurasa wa 3 fungu la nne lilitamka hivi, “...hivi sasa katika Afrika ni kwamba hakujawa na wananchi wa nchi yoyote ya Afrika ambayo wamekwisha fikia kiwango cha ukombozi halisi.
Afrika bado ni bara la watu waliyomo katika unyonge wa kunyonywa na kunyanyaswa. Ndio kusema kwamba vyama vya siasa vya kimapinduzi katika nchi za Afrika zinazojitawala, kama vile TANU, bado vingali ni vyama vya ukombozi.”
Ni miaka takriban 41 (sasa) tangu andiko hili litolewe; Tanzania tungali watumwa na tumeshindwa kufanya mapinduzi ya fikra. Inawezekana msomaji ukashangaa kwa nini naandika hapa kwamba, “Tanzania ni watumwa wa fikra.”
Utumwa wa fikra ni hali inayompata mtu anayejiona yupo huru huku mawazo yake yamefungwa kwenye kutawaliwa. Kwa mtaji huu, anaendelea kuwa mtumwa wa kuwatumikia wakoloni kiuchumi, kisiasa, na kijami kama wakala anayetumika kwa masilahi ya kibinafsi.
Wengi wa watumwa wa fikra ni wale wanaopewa nafasi za uongozi (kama dhamana) huku wakitumia nafasi hizo kwa utashi wa mabeberu (na wastakabari) wanyonyaji.
Viongozi wengi wa nchi za Afrika, pamoja na Tanzania, ni watumwa wa fikra na wanatawala kama mawakala wa mabeberu.
Uhuru umeuzwa kwa utashi wa viongozi wachache waliyejipa mamlaka ya kutawala wananchi wasiyekuwa na satwa kwa misingi ya utawala wa demokrasia za kijeshi.
Kama lilivyoainisha Azimio la Arusha (05/02/1967) kwamba, “Tumeonewa kiasi cha kutosha, tumenyeonywa kiasi cha kutosha, tumepuuzwa kiasi cha kutosha. Unyonge wetu ndio uliyotufanya tuonewe, tunyonywe, na kupuuzwa. Sasa tunataka kufanya mapinduzi... .”
Hakuna mapinduzi ya fikra yaliyoambatana na kuwashwa mwenge uliyodhamiria kuleta matumaini mapya kwenye fikra za wananchi baada ya uhuru!
Uhuru wa bendera (kwa kuiteremsha Union Jack na kupandisha bendera ya uhuru wa Tanganyika) hakukuleta saada (manufaa) ya moja kwa moja katika kuwaondoa wananchi katika mawazo ya kutawaliwa.
Viongozi waliyechukua nafasi za wakoloni wamegeuka mbwa-mwitu (waliyevalia ngozi za kondoo) na kuendesha ujambazi wa kiserikali.
Uongozi wa kisiasa na unaotawala uendeshaji wa shughuli za serikali (kuu na za mitaa) umekuwa ukijivika sura ya ubinadamu kwa kutangaza thamani ya uhuru, haki na usawa ilhali kwa wakati huohuo menejimenti ya uchumi, siasa na jamii ikiwekwa rehani kwa mabeberu na wanyonyaji wa kigeni kwa njia ya ubinafsishaji, unyang’anyi na ujambazi wa kiserikali (kleptocracy).
Uhuru umepoteza maana; na matumaini yaliyodhaniwa kupatikana baada ya uhuru yamegeuka machungu ya kutawaliwa kiuchumi, kijamii na kisiasa na mawakala (na makuwadi) wa utandawazi wanaolipwa na wanyonyaji kwenye siasa za kimataifa. Hivi ndivyo thamani ya uhuru ilivyopotea na kwa jinsi hiyo; nadhani, kama dhana chanya, mwenge umepoteza thamani pia!
Hata kama utabaki kuwa alama ya vijana wa CCM, alama ya Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), alama kwenye baadhi ya vyo vikuu na taasisi za umma (kama Chuo Kikuu Mlimani, Chuo Kikuu Mzumbe, na kadhalika) bado nadhani kuwepo kwake kwenye “alama” hizo kutabaki kama historia iliyokosa mashiko kwa vile falsafa ya mwenge ilikuwa kuleta matumaini kwa wananchi. Kama matumaini ya uhuru hayakufikiwa leo (takriban miaka 50 ya uhuru) yatafikiwa lini?
Hata wale waliyebudni dhana ya “tumethubutu, tumeweza na tunasonga mbele” sijui walifikiria nini na kwa nini? Sijapa majibu ya dhana hii! Inawezekana, kwa utashi wa waliyebuni falsafa ya Miaka ya 50 ya Uhuru, wana hoja makini na yenye ithibati; muda utatueleza juu yake.
Nukta ya pili kwenye tamko la kuwasha mwenge ni upendo; kama dhana pana na yenye hitajio la uchambuzi angavu. Mwenge ulisadikiwa uwashwe ili pale penye chuki pawe na upendo! Upendo uliolengwa hapa sidhani kama ni ule wa “mapenzi” ya ngono uzembe ambapo kwenye mikesha ya “mbio za mwenge” vijana wa kike na kiume wanajimwaga kama wapo kwenye “fiesta” huku wanakula na kuponda raha kana kwamba wapo Manhattan (New York)! Upendo uliyodhamiriwa na uwashwaji wa mwenge ni hali angavu ya thamani ya utu na ubinadamu wa kujali, kuhurumiana, kusaidiana katika hali zote, kushirikiana katika uzalishaji mali na kugawana pato la taifa kwa njia za uhuru, haki na usawa. Upendo uliyotakiwa ni kujitolea kwa masilahi ya watu wengine.
Dhana ya upendo ililenga kauli mbiu ya “kila mtu anastahili heshima ya kutambuliwa na kuthaminiwa utu wake.” Leo uongozi wa kisiasa umesahau dhana hii; na wananchi waliyo wengi wanaishi kwa chuki; na kuchukiana imekuwa ndio itikadi ya vyama na wanasiasa. Wanasiasa wanachukiana; wanahasimiana, na hata kutaka kuuana kwa sumu na mitego mingine ya kisiasa! Chuki imefanywa sehemu ya siasa kwa wanasiasa na wananchi wa kawaida. Hakuna upendo wa kweli baina ya watu wa jinsi moja na au jinsi tofauti; watu wamekuwa kama wanyama wanaokula nyama na wale wanaokula nyasi: tunawindana kwa kuviziana katika kutafuta ulipizaji wa visasi, kutesana, na kuuana.
Mateso yanayotokana na chuki za kiwendawazimu yamemfanya binadamu kuwa kama ‘shetani’ mwenye jicho moja au “milihoi” au “popo-bawa” au popo-mnyonya damu (vampire) kwa kutamani damu za wahanga. Binadamu amekuwa mtu wa chuki na roho (ya shetani) anayetamani kuua na au kutesa binadamu wengine! Huyu ndiye binadamu aliyebadilika roho na kuchukua maisha ya kihayawani kwa kutamani kuzima kiu yake ya ufisadi wa kishenzi kwa kukandamiza uhuru, haki na usawa wa watu wengine pasipo haki na makusudi ya uumbwaji wake kwa mujibu wa sheria, kanuni na taratibu za kimaumbile. Chuki inayowachukua wanasiasa na watu wengine ndio inayozaa mauwaji na utesaji wa watu wasiyekuwa na hatia (rejea: mauwaji ya albino na vikongwe; mauwaji ya watu wasiyo na hatia; na mateso yanayofanywa kwa watu kiakili, kimwili na kisaikolojia).
Binadamu amejaa tamaa na uchu wa kihayawani zaidi kuliko wakati wa kabla na baada ya miaka ya mwanzo ya uhuru. Binadamu waliyekabidhiwa uongozi wa chama na serikali na hata kwenye baadhi ya vyama vya siasa, kijamii na kiuchumi wamekuwa walafi, wenye choyo na roho zenye inda na ila ya kutamani kupata zaidi kwa njia zisizokuwa halali!
Haya na mengine wanayoyaficha kwenye nafsi zao huwapa kiburi na kujenga mazingira ya chuki baina ya watu wenye nacho na wale masikini waliyo wengi. Chuki baina ya wenye nacho na wasiyo nacho (masikini wa kutupwa) hujenga matabaka ya kijamii ambayo kwa sehemu kubwa ndio yanayoongeza upogo (tofauti) baina ya watu wenye hali ya juu kimaisha na watu wa hali ya chini kimaisha. Kuwepo kwa mfumo huu wa maisha unaotokana na roho ya chuki; ndivyo kunavyochochoea uhalifu na vurugu za kijamii.
Nukta ya tatu na ya mwisho; ni heshima! Kama nilivyogusia hapo kabla, binadamu anahitaji heshima ya kutambuliwa na kuthaminiwa utu wake. Heshima ya binadamu inatokana na kazi. Hata hivyo, sote (mimi na wewe) ni mshahidi kwamba, “heshima na utu wa sehemu kubwa ya wananchi wa Tanzania imetoweka kwa kukosa uhuru, haki na usawa katika kazi.” Kazi (ajira) kwa wananchi wengi wa Tanzania ni kilimo, siyo? Jibu la moja kwa moja ni: ndiyo!
Kama ndiyo; hebu tukitazame kilimo chetu, bado ni cha jembe la mkono (kiserema) na kutegemea mvua kwenye mashamba yasiyokuwa na uwezo wa kuzalisha ziada. Tumekuwa hata wakati mwingine tukitegemea chakula cha msaada kutoka kwa mikoa yenye ziada ya chakula (kwa usaidizi wa serikali) au hata kuomba misaada (kama ilivyowahi kutokea miaka ya 1970).
Heshima ya wananchi wa vijijini imepungua kwa vile baada ya kutelekezwa sera ya ujamaa vijijini (miaka ya 1970) wamekuwa kama wakimbizi kwenye nchi yao. Maisha magumu na msoto huku wengi wakipoteza uwezo wa kuzalisha na kujikuta wakitumikishwa kwenye mashamba na miradi ya wawekezaji waliyewekeza kwenye ardhi ya wananchi na au hata kuwapora ardhi yao kwa kisingizio cha uwekezaji na au ubinafsishaji. Wananchi wamebaki watumwa kwa kufanyishwa kazi za kijungu-jiko (kishumbutu) ilhali faida ya kazi ikivunwa kwa wingi (wa faida) na wawekezaji.
Wananchi wamefanywa raia daraja la pili na la tatu. Wawekezaji wamepewa haki zaidi (exclusive rights) na hata wakati mwingine wanafanya wapendavyo; kama vile kuchafua vyanzo vya maji vya wananchi kwa kemikali za sumu na hata kuwaua pale wanapodhaniwa kuvuka mipaka ya miradi ya wawekezaji.
Kwa hali hizi tatu zilizojadiliwa na kuwekwa hapa (japokuwa kwa muhtasari sana); nadhani ni sahihi kabisa kudhani kwamba, “mwenge wa uhuru umepoteza maana yake ya kifalsafa.” Kama alama, basi imebaki alama isiyokuwa na athari zilizokusudiwa kwenye tangazo la tarehe 22, Oktoba 1959 lilitolewa na Mwalimu Nyerere. Mwenge wa uhuru umebaki kuwa sehemu ya “programu ya kampeni” kwa chama tawala kwa vile mara zote vijana wake ndio wanaopewa nafasi ya kushiriki kwenye harakati zake (na ndio wanaotumia alama hiyo).
Jitihada za makusudi zinazofanywa na makada mbalimbali wa vyama mbaimbali vya siasa juu ya kuhuisha moyo wa kizalendo kwa kuutumia mwenge wa uhuru zimekuwa zikizimwa na wanasiasa waliyomo ndani ya mfumo wa utawala msonge kwa kile kinachodaiwa kwamba, “mwenge ni alama yao na kamwe hawawezi kukubaliana na mawazo mbadala juu yake.”
Hivi ndivyo ilivyo; na ndivyo baadhi ya wanasiasa vijana, wakongwe na vigogo wanavyodhani na kutaka hali hiyo iendelee milele kwa kuwa kwa hali hiyo na mazingira yalivyo chama chao kinanufaika na mfumo wa nchi kukosa (1) matuamaini ya uhuru (2) upendo na (3) heshima ya binadamu. Nchi inaendesha kama shmaba la wanyama ilhali kuna kla sababu ya maisha yenye staha na yenye hadhi ya utu na heshima ya binadamu.
Mwisho, wakati umefika sasa; tukubali kwamba, “mbio za mwenge zimebaki kuwa udhalilishaji wa falsafa na dhana ya uhuru.” Kwa iuwa hakuna uhuru mahali ambapo hapana matumaini; hakuna uhuru mahali pasipokuwa na upendo; na hakuna uhuru mahali pasipokuwa na heshima ya binadamu.
Pale mwanzo palipokuwa na Azimio la Arusha wananchi wa Tanzania walikuwa na hakika ya kufanya mapinduzi ya fikra kwa kukataa kuonewa, kunyonywa, kupuuzwa na kudharauliwa; baada ya kupuuzwa Azimio la Arusha na kuchochewa kwa moto wa ujasiriamali wa kisiasa na kuwafanya wanasiasa wa chama tawala kujiingiza moja kwa moja kwenye uwakala wa kuharibu mujtamaa wa ujenzi wa jamii ya watu waliyo sawa na huru.
Wanasiasa walafi wameharibu nchi na kuifanya kama “shamba la bibi.” Vijana wamegeuzwa mtaji wa kisiasa kwa wanasiasa vigogo kuwatumia kwa kigezo cha mwenge wa uhuru kueneza propaganda na mwisho wake sehemu ya vijana wanaoshiriki kwenye kukimbiza mwenge hupewa nafasi za utendaji kama fadhila ya utumishi wao kwenye kueneza chuki ya maangamizo ya uharibifu wa shakhsiya ya vijana wengi kwa vile hakuna matumaini ya vijana wasiokuwa na kazi mahsusi kwenye maisha yao ya leo na kesho.
Hakuna njia nyepesi kwa vijana na kizazi cha Tanzania isipokuwa kukubali mapinduzi ya fikra. Kwa elimu yenye manufaa ndipo vijana na kizazi cha Tanzania kinaweza kujikomboa na uzezeta wa kutumiwa kama daraja na wanasiasa walafi na wenye uchu wa kutawala kifisadi

EmoticonEmoticon