Marufuku hiyo ilitangazwa Jumatano (13 Septemba) ambapo msemaji wa polisi, Charity Charamba, alisema itaendelea kutekelezwa hadi mripuko wa kipindupindu utakapodhibitiwa. "Wananchi wanatakiwa kufuata maagizo haya, kwani itasaidia kukabili maambukizi ya ugonjwa huu," alisema Charamba.
Kiongozi wa upinzani nchini Zimbabwe, Nelson Chamisa, alikuwa amepanga kuandaa mkutano siku ya Jumamosi (15 Septemba) ambapo alitarajiwa kujiapisha, wiki tatu baada ya Rais Emmerson Mnangagwa kuapishwa kufuatia uamuzi wa mahakama uliouidhinisha ushindi wake katika kesi iliyowasilishwa na Chamisa kupinga matokeo ya uchaguzi.
Hata hivyo, msemaji wa Chamisa, Nkululeko Sibanda, hakutoa taarifa yoyote baada ya marufuku hiyo kutolewa. Chamisa alitembelea vituo vya afya ambapo wagonjwa wa kipindupindu walikuwa wakitibiwa jana na kuwataka maafisa wa afya na serikali kushirikiana. Aidha aliutaka Umoja wa Mataifa kutoa usaidizi kwani suala hilo ni zaidi ya dharura, na kulitaja kuwa janga la kitaifa.
Vile vile, polisi walisema wamepiga marufuku uuzaji wa vyakula katika maeneo mbalimbali kwenye mitaa miwili iliyoathirika zaidi pamoja na mji mkuu, Harare.
Kwenye taarifa iliyotolewa na polisi, jeshi hilo lilisema lingeimarisha doria mjini humo na kuhakikisha kwamba marufuku hiyo "inazingatiwa kwa ukamilifu na kila mmoja bila woga au upendeleo."
Waziri wa afya alisema wakati wa kikao cha idara mbalimbali za serikali kuwa jumla ya watu 3,000 walikuwa wameambukiwa kipindupindu na ugonjwa huo umetajwa kusambaa nje ya mji.
Mripuko mkubwa zaidi wa kipindupindu ulitokea nchini humo mwaka 2008 ambapo watu 4,000 walifariki dunia na takriban 100,000 kuambukizwa, kwa mujibu wa data za wizara ya afya.
Taifa la Zimbabwe bado linajaribu kujitibu masaibu ya mageuzi yaliyoshuhudiwa mwaka uliopita, wakati Robert Mugabe alipoondolewa madarakani na aliyekuwa naibu wake Emmerson Mnangagwa kuteuliwa kuwa rais. Rais Mnangangwa aliahidi kuboresha huduma za umma, zikiwemo za afya