Msanii mkongwe na maarufu nchini Tanzania na Afrika Mashariki Amri Athuman maarufu Mzee Majuto amefariki dunia wakati akipokea matibabu kwenye hospitali ya Taifa Muhimbili iliyopo Dar es Salaam Tanzania.
Muigizaji huyo veterani alilazwa katika chumba cha wagonjwa mahututi kabla ya kufariki kwake.
Taarifa ya ikulu imesema King Majuto amefariki dunia majira ya saa 1:30 Jioni katika Hospitali ya Taifa Muhimbili alikokuwa akipatiwa matibabu.Tayari watu maarufu ndani na nje ya Tanzania wametuma salamu za rambirambi kwa familia yake kupitia mitandao ya kijamii, miongoni mwao Rais wa Tanzania John Magufuli.
Rais Magufuli amesema King Majuto atakumbukwa kwa mchango wake mkubwa na wa muda mrefu alioutoa kupitia sanaa ya uigizaji na uchekeshaji, ambapo alishiriki kuelimisha jamii, kuendeleza na kukuza sanaa na kuunga mkono juhudi za chama na Serikali katika kuhimiza maendeleo.
"King Majuto alikuwa kielelezo cha safari ndefu ya sanaa kwa nchi yetu, kwa muda wote amedhihirisha kipaji, ujuzi na uwezo wa hali ya juu katika uigizaji na uchekeshaji na hivyo kuwa kipenzi cha Watanzania na wasanii wenzake, hatutasahau ucheshi wake, upendo na uzalendo kwa nchi yake wakati wote wa uhai wake," amesema Rais Magufuli.
Kiongozi huyo wa nchi alimjulia hali msanii King Majuto alipokuwa amelazwa katika hospitali ya Tumaini jijini Dar es salaam 31 Januari, 2018.
Kiongozi wa chama cha upinzani cha ACT Wazalendo, ambaye pia ni mbunge wa Kigoma-Ujiji Zitto Kabwe amesema: "Nimepokea Taarifa ya msiba wa Mzee Majuto kwa masikitiko makubwa sana. Tumshukuru Mola kwa uwezo wake na kuwaombea wafiwa kwa mola awape subra."
Msanii maarufu wa bongo fleva Naseeb Abdul akijulikana zaidi kama Diamond Platnumz, ameandika kuwa Mzee Majuto ni mfalme ambae ataishi mioyoni mwa wengi daima.
Msanii Ali Kiba naye ameandika: "Ewe Mwenyezi Mungu hakika Mzee Wetu Amri Bin Athuman (King Majuto) yuko katika dhima yako na kamba ya ujirani wako, basi mkinge na fitina ya kaburi na dhabu ya moto nawe ndiwe mstahiki wa utekelezaji na ukweli msamehe na umrehemu hakika Wewe ni mwingi wa kusamehe, mwingi wa kurehemu. Amin."
EmoticonEmoticon