SERIKALI KUONGEZA ASKARI WANYAMAPORI KWA AJILI YA KUKABILIANA NA WANYAMA WAKALI NA WAHARIBIFU

HOJA NEWS BLOG

Na. Anangisye Mwateb- Dodoma

Serikali inatarajia kuongeza askari wanyamapori wa vijiji ikiwa ni mkakati wa muda mfupi wa kupambana na changamoto ya wanyamapori wakali na waharibifu kwenye maeneo yanayopakana na hifadhi za taifa, hifadhi za misitu na mapori ya akiba.


Haya yamesemwa na Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii Mhe. Dunstan Kitandula wakati akijibu swali la Mhe. Hassan Zidadu Kungu Mbunge wa Tunduru aliyetaka kujua lini Serikali itaweka mpango madhubuti unaotekelezeka wa kukabiliana na wanyama wakali wakiwemo tembo ambao wamekuwa wakisababisha vifo vingi na kuleta hasara ya mazao kwa Wananchi wa Tunduru na maeneo mengine nchini.

Mhe. Kitandula amesema Wizara ya Maliasili na Utalii imechukua hatua mbalimbali ikiwemo kutoa elimu kwa wananchi kuhusu tabia za wanyamapori na mbinu za kujikinga na wanyamapori wakali na waharibifu ambapo vijiji 83 vyenye jumla ya wananchi 50,284 wa Wilaya ya Tunduru wamepatiwa elimu.

Vilevile wizara imekuwa ikifanya doria za udhibiti wa wanyamapori wakali na waharibifu; kujenga vituo vya askari kwenye makazi ya wananchi ili kuwasogeza askari karibu na maeneo yenye changamoto.

Mhe. Kitandula aliongeza kuwa kwa Wilaya ya Tunduru wizara imejenga kituo cha askari cha kudumu katika kijiji cha Chingulungulu na kituo cha askari cha muda katika kijiji cha Mbesa lakini pia imejenga vizimba vya kuzuia mamba wasidhuru wananchi wanapotumia maji ya mito au maziwa. 

Aidha wizara imeandaa mfumo wa kielektroniki ili kuimarisha mfumo wa ukusanyaji na utunzaji wa taarifa za matukio ya wanyamapori wakali na waharibifu.

Vilevile Mhe. Kitandula alisema kuwa ili kuhakikisha usalama wa Wananchi wa Wilaya ya Tunduru pamoja na mali zao dhidi ya tembo, Wizara inaendelea kuchukua hatua mbalimbali za udhibiti ikiwa ni pamoja na ununuzi wa magari mawili, pikipiki tatu, ndege zisizo na rubani tano. 

Aidha, mafunzo kwa Askari Wanyamapori wa Viijiji yamepangwa kutolewa mwanzoni mwa mwaka 2024 kwa ajili ya kuongeza nguvu katika udhibiti wa tembo.




Pia serikali inaendelea kukamilisha kanuni za kifuta jasho na kifuta machozi ili kiendane na hali halisi na uharibifu unaofanywa na wanyama wakali na waharibifu.

Share this

Related Posts

Previous
Next Post »