Na. Anangisye Mwateba-Dodoma
Wananchi wa Kisiwa cha Maisome kilichopo katika ziwa Victoria wilayani Sengerema watamegewa hekta 2943.8 kutoka katika Hifadhi ya Msitu wa Maisome kwa ajili ya Malisho ya Mifugo.
Haya yamesemwa na Naibu waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Dunstan Kitandula alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Jimbo la Buchosa, Mhe. Eric James Shigongo aliyetaka kujua lini Serikali itawamegea eneo Wananchi wa Visiwa vya Maisome katika Hifadhi ya Kisiwa cha Maisome.
Mhe. Kitandula aliongeza kuwa Serikali imechukua hatua katika kutekeleza maelekezo ya Baraza la Mawaziri kwa kufanya mapitio ya mpaka wa msitu wa hifadhi ya Maisome ambapo hekta 2,943.8 zitatolewa kwa wananchi na eneo hilo kubakiwa na hekta 9,319.2.
”Kwa sasa taratibu za kubadili mpaka kisheria na kupata ramani mpya zinaendelea. Mara zoezi hilo litakapokamilika Mheshimiwa Mbunge pamoja na Wananchi watajulishwa ambapo watakuwa na muda wa siku 90 kutoa maoni yao kabla ya tangazo rasmi la kutangaza eneo jipya la hifadhi baada ya mabadiliko niliyoyasema hapo juu” aliongeza Mhe. Kitandula.
Katika hatua nyingine Mhe. Kitandula alisema kuwa katika kutatua changamoto za mwingiliano wa shughuli za uhifadhi na zile za kibinadamu, Serikali iliwasilisha taarifa ya umuhimu wa kumega hifadhi hiyo kama sehemu ya utatuzi wa migogoro ya vijiji 975.
EmoticonEmoticon