Anangisye Mwateba-Dodoma
Serikali iko kwenye mchakato wa kuweka malipo ya wapagazi, waongoza watalii na wapishi katika mlima kilimanjaro kuwa kisheria.
Hayo yamesemwa na Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii Mhe. Dunstan Kitandula(MB) wakati akijibu swali la Mhe. Dkt. Charles Stephen Kimei, Mbunge wa Vunjo ambaye alitaka kujua lini Serikali itafanya mapitio ya viwango vya malipo ya ujira kwa wapagazi, wapishi na waongoza watalii katika Hifadhi ya Mlima Kilimanjaro.
Mhe. Kitandula alifafanua kuwa Serikali inatambua changamoto ya viwango vya malipo ya ujira kwa wapagazi, wapishi na waongoza watalii katika Hifadhi ya Mlima Kilimanjaro.
Aidha, katika kutatua changamoto hizo, Wizara kwa kushirikiana na Vyama vya mawakala wa utalii yaani waajiri imeanza kutekeleza mikakati mbalimbali kwa ajili ya kufanya maboresho ya viwango hivyo vya malipo ya ujira.
‘‘ Wizara imefanya kikao na Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu na kujadili kuhusu viwango vya ujira kwa wapagazi, wapishi na waongoza watalii“ aliongeza Mhe. Kitandula
Mhe. Kitandula aliongeza kuwa Wizara kwa kushirikiana na Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu inatarajia kufanya kikao kazi na wadau hao na waajiri wao kwa lengo la kupendekeza viwango stahiki ili viweze kuwasilishwa katika Bodi ya Utatu yenye dhamana ya kumshauri Waziri mwenye dhamana ili makubaliano hayo yawe ya kisheria.
EmoticonEmoticon